
MWAIPAYA AIPONGEZA KCJE KWA MAFANIKIO MAKUBWA SEKTA YA KOROSHO

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, ameipongeza Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Limited kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kuimarisha sekta ya korosho nchini, akisema taasisi hiyo imekuwa nguzo muhimu ya kuinua uchumi wa wakulima na kuimarisha Ushirika.
Akizungumza wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa Tano wa KCJE Limited, uliofanyika Julai 15, 2026 mkoani Mtwara, Mwaipaya alisema taasisi hiyo imeonyesha mafanikio ya kipekee katika kuratibu huduma muhimu kwa wakulima, hatua inayochochea ongezeko la tija na ubora wa zao la korosho.
“KCJE imekuwa mfano wa kuigwa katika Ushirika, Mafanikio mliyoyapata yanaonesha wazi kuwa mna uongozi imara, mshikamano na maono ya pamoja ya kuwaletea wakulima maendeleo,” alisema.
Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuimarika kwa upatikanaji wa pembejeo za kilimo, vifaa vya kufungashia mazao, mizani ya kidijitali na viuatilifu, huduma ambazo zimewasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na ubora wa korosho zao.
Mwaipaya alisema hatua ya KCJE kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha na utawala bora imeongeza imani ya Serikali, wanachama na wadau mbalimbali, na kuifanya taasisi hiyo kuwa miongoni mwa Vyama vya Ushirika vinavyoaminika zaidi nchini.
Alisema mafanikio hayo yanakwenda sambamba na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kuboresha mazingira ya sekta ya Korosho kupitia sera rafiki na uwekezaji katika mnyororo wa thamani.
Aidha, aliipongeza KCJE kwa kuendelea kubuni mbinu mpya za kuongeza mapato, kuwekeza katika teknolojia na kuimarisha ushirikiano na taasisi za kifedha pamoja na wadau wa maendeleo, hatua alizosema zinaiweka taasisi hiyo katika nafasi nzuri ya ushindani.
Hata hivyo, aliwataka viongozi wa KCJE kuendeleza mafanikio hayo kwa kuzingatia uwajibikaji, uwazi na uadilifu katika usimamizi wa rasilimali, akisisitiza kuwa uaminifu ndio msingi wa mafanikio ya taasisi yoyote ya Ushirika.
“Endeleeni kulinda imani ya wakulima na Serikali kwa kuhakikisha kila hatua mnayochukua inaleta tija na maendeleo ya kweli kwa wanachama wenu,” alisisitiza.
Akihitimisha, Mwaipaya aliwapongeza Mwenyekiti wa Bodi, menejimenti na wanachama wa KCJE kwa kujenga taasisi imara na yenye mafanikio, akisema Serikali itaendelea kushirikiana nao ili kuifanya sekta ya korosho kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa.
Habari Zinazohusiana
MakalaKOROSHO TANI 49,093 ZENYE THAMANI YA ZAIDI BILIONI 160 ZAUZWA WIKI YA KWANZA YA MINADA
Jumla ya kilo 49,093,143 sawa na tani 49,093.143 za korosho ghafi zenye thamani ya shilingi bilioni 160 zimeuzwa katika minada minne iliyoendeshwa na Vyama Vikuu vya Ushirika vya mikoa ya Lindi na Mtwara, katika wiki ya kwanza ya msimu wa mauzo ya korosho wa mwaka 2026/2027. Minada hiyo ilianza Oktoba 12 na 13, 2026, kupitia […]
Soma zaidi
MakalaKCJE KUSAMBAZA MAGUNIA MILIONI 9.3 MSIMU WA KOROSHO WA 2026/2027
Meneja Mkuu wa Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Limited, Mohamed Mwinguku, amesema KCJE imejipanga kuhakikisha hakutakuwa na changamoto ya upatikanaji wa magunia katika msimu wa mauzo na masoko ya korosho wa 2026/2027. Mwinguku amesema makadirio ya uzalishaji wa korosho kwa msimu huo ni tani 750,000, huku mahitaji ya magunia yakikadiriwa kufikia zaidi ya milioni 9.35. […]
Soma zaidi
MakalaTANGAZO LA ZABUNI YA PEMBEJEO ZA KILIMO
Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Cooperative Joint Enterprise Limited (KCJE Ltd), Odas Mpunga anatangaza zabuni Na. KCJE/2027/2028/G/02 kwa ajili ya ununuzi wa Pembejeo za Kilimo. Waombaji wanatakiwa kuwasilisha zabuni zao katika Ofisi za KCJE zikiwa na nakala halisi moja (1) na kivuli mbili (2) pamoja na kulipa ada isiyorejeshwa ya Sh5 milioni kupitia akaunti ya […]
Soma zaidi